Bodi ya Ushauri Yafanya Ziara Chuo cha Maji, Dar es Salaam
Published on: 13th January, 2025
Dar es Salaam, 5 Oktoba 2024 - Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha
Maji leo wamefanya ziara rasmi katika Chuo cha Maji, Dar es Salaam,
ambapo walikagua maendeleo ya miradi mbalimbali. Ziara hiyo ilikuwa na
lengo la kutathmini hatua zilizofikiwa katika ujenzi na ukarabati
unaoendelea chuoni ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa
viwango vya ubora vinavyokubalika.
Katika ziara hiyo, wajumbe
walipata nafasi ya kutembelea jengo jipya la chuo, linalojulikana kama
Maji House, ambalo liko katika hatua za mwisho za kukamilika. Wajumbe,
wakiwa wameongozana na menejimenti ya chuo, walikagua ofisi na maeneo
mengine yaliyopo kwenye jengo hilo jipya ili kupata uelewa wa jinsi
litakavyoongeza ufanisi wa shughuli za kiutawala na kimasomo.
Aidha,
wajumbe wa bodi walitembelea ujenzi wa maktaba mpya na kuona maendeleo
ya ukarabati wa madarasa ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi
Desemba mwaka huu. Katika ziara hiyo, wajumbe walipata nafasi ya
kukutana na mkandarasi anayesimamia mradi huo na kuzungumzia changamoto
mbalimbali zinazochelewesha ukamilishaji wa ujenzi huo.
Wajumbe
hao walitoa mapendekezo yatakayohakikisha ujenzi huo unakamilika kwa
muda uliopangwa na kwa ubora unaohitajika. Miradi hii ya ujenzi na
ukarabati itatoa mazingira bora ya kujifunzia na kufanya kazi, na hivyo
kuimarisha uwezo wa chuo katika kuzalisha wataalamu wa maji wenye ujuzi
na uzoefu wa kutosha kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye sekta
ya Maji.