CHUO CHA MAJI KUJA NA UBUNIFU WA ATM ZA MAJI
Published on: 22nd April, 2025
Mkuu wa Chuo cha Maji, Dkt. Adam Karia, amesema kuwa chuo hicho
kimeendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kwa kuzalisha wataalam
waliobobea katika sekta ya maji, hatua inayosaidia kufanikisha malengo
ya maendeleo endelevu (SDGs), hususan lengo namba sita linalohusu
upatikanaji wa maji safi na salama.
Akizungumza katika Kongamano
la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika Ukumbi wa
Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Jumatano Januari 29, 2025, Dkt.
Karia ameeleza kuwa chuo hicho kimefanikiwa kubuni teknolojia
mbalimbali, ikiwemo mashine za ATM za maji ambazo tayari zinatumika.
Amebainisha
kuwa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye ni Mgeni Rasmi wa kongamano
hilo, kuhusu kuhakikisha mashine hizo zinawafikia wananchi wa vijijini
yamepokelewa, na juhudi zinaendelea kuhakikisha upatikanaji wa maji safi
unarahisishwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Aidha, Dkt. Karia
amezungumzia Mfumo wa Usimamizi wa Uvujifu wa Maji -Integrated Leakage
Management System (ILMS) ambao ni ubunifu wa wanafunzi na walimu wa Chuo
cha Maji. Amesema mfumo huo umeonesha mafanikio makubwa katika
kupunguza upotevu wa maji (Non-Revenue Water), hali iliyosaidia kuokoa
fedha zilizokuwa zinapotea kutokana na upotevu wa maji. Kwa sasa, mfumo
huo unatumika katika mikoa kama Dodoma, Tanga na eneo la Igunga-Tabora,
huku ukiwa umeonesha mafanikio makubwa visiwani Zanzibar.
Amesema
kuwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, ameagiza kuhakikisha mfumo
huo unatekelezwa kikamilifu katika kisiwa cha Pemba na mikoa yote ya
Unguja.
Kongamano hilo, ambalo Mgeni Rasmi ni Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, limeanza
Januari 29, 2025, na linatarajiwa kufikia tamati Januari 31, 2025.