News

CHUO CHA MAJI KUJA NA UBUNIFU WA ATM ZA MAJI

Mkuu wa Chuo cha Maji, Dkt. Adam Karia, amesema kuwa chuo hicho kimeendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kwa kuzalisha wataalam waliobobea katika sekta ya maji, hatua inayosaidia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), hususan lengo namba sita linalohusu upatikanaji wa maji safi na salama.

Akizungumza katika Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Jumatano Januari 29, 2025, Dkt. Karia ameeleza kuwa chuo hicho kimefanikiwa kubuni teknolojia mbalimbali, ikiwemo mashine za ATM za maji ambazo tayari zinatumika.

Amebainisha kuwa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye ni Mgeni Rasmi wa kongamano hilo, kuhusu kuhakikisha mashine hizo zinawafikia wananchi wa vijijini yamepokelewa, na juhudi zinaendelea kuhakikisha upatikanaji wa maji safi unarahisishwa kwa wananchi wa maeneo hayo.

Aidha, Dkt. Karia amezungumzia Mfumo wa Usimamizi wa Uvujifu wa Maji -Integrated Leakage Management System (ILMS) ambao ni ubunifu wa wanafunzi na walimu wa Chuo cha Maji. Amesema mfumo huo umeonesha mafanikio makubwa katika kupunguza upotevu wa maji (Non-Revenue Water), hali iliyosaidia kuokoa fedha zilizokuwa zinapotea kutokana na upotevu wa maji. Kwa sasa, mfumo huo unatumika katika mikoa kama Dodoma, Tanga na eneo la Igunga-Tabora, huku ukiwa umeonesha mafanikio makubwa visiwani Zanzibar.

Amesema kuwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, ameagiza kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa kikamilifu katika kisiwa cha Pemba na mikoa yote ya Unguja.

Kongamano hilo, ambalo Mgeni Rasmi ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, limeanza Januari 29, 2025, na linatarajiwa kufikia tamati Januari 31, 2025.

Posted on 31st January, 2025