News

MKUU WA WILAYA YA UBUNGO AFANYA ZIARA CHUO CHA MAJI

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mheshimiwa Hashim Abdallah Komba, amefanya ziara katika Chuo cha Maji leo tarehe 12/04/2023 na amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Chuo, Dkt. Adam O. Karia pamoja na menejimenti ya Chuo hiko.
Kwenye mazungumzo hayo, Mkuu wa Wilaya alimshukuru Mkuu wa Chuo kwa mapokezi mazuri na kuomba Chuo kuendelea kutoa ushirikiano kwake na kwa watendaji wake wa Wilaya ya Ubungo kwa maslahi mapana ya Watanzania katika jukumu zima la kuzalisha wataalam wa sekta adhimu ya maji Nchini.
Miongoni mwa mambo aliyoyasema ni pamoja na Chuo kutoa taarifa za miradi mbalimbali inayotekelezwa chuoni kwa fedha zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo fedha za ukarabati wa madarasa na ujenzi wa maktaba utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 5.9 ( mradi huo unatarajia kuanza tarehe 24/04/2023) ambapo Mkuu wa Wilaya ameahidi kuwa miongoni mwa Viongozi watakaoshiriki hafla ya kukabidhi eneo la ujenzi kwa wakandarasi wanaohusika na utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo.

Vilevile, Mheshimiwa Hashim Abdallah Komba alisisitiza suala la ulinzi na usalama. Yeye kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ubungo alisema mambo matatu yanapaswa kufanyika. Kwanza, Chuo kitoe huduma za ushauri wa kisaikolojia kwa wanafunzi ili kupunguza wimbi la wanafunzi wanaokata tamaa wanapokutana na changamoto mbalimbali na kupelekea kuwa vichaa au kupoteza maisha kwa kujinyonga. Jambo la pili, Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuimarishwa kwa ulinzi chuoni ili kubadiliana na matukio ya kihalifu na uvunjifu wa amani na jambo la mwisho na kwa umuhimu wake, Mkuu wa Wilaya amekitaka Chuo kutoa taarifa za uhalifu kituo cha Polisi pindi uhalifu unapotokea.

Kabla ya kumaliza ziara yake, Mkuu wa Wilaya alipata nafasi ya kutembelea Maabara za Chuo cha Maji na kujionea vifaa vilivyopo na tafiti mbalimbali zinazofanyika. Pia alitembelea mabweni yaliyokarabatiwa, pamoja na ujenzi wa madarasa unaoendelea. Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alipongeza Chuo cha Maji kwa kazi kubwa inayofanyika na kusisitiza kuendelea kutunza mazingira na kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa kwenye kampeni ya utunzaji mazingira ya "Safisha Pendezesha Dar es Salaam".

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo, Dkt. Adam O. Karia, alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa ziara hiyo na kumkaribisha tena kutembelea Chuo cha Maji. Vilevile, Mkuu wa Chuo alielezea changamoto zinazokabili Chuo ikiwemo uvamizi wa eneo la Chuo unaofanywa na wafanyabiashara wadogo pamoja na uharibifu wa miundombinu unaofanywa na wachimbaji wa mchanga katika Mto Ng'ombe. Mkuu wa Wilaya aliahidi kushirikiana na Chuo kutatua changamoto hizo.

Posted on 12th April, 2023