News

​Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa H. Aweso, amefanya kikao kazi Chuo cha Maji

Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa H. Aweso, amefanya kikao kazi na watumishi wa Chuo cha Maji pamoja na wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Sehemu ya Uchimbaji Visima. Kikao kazi hicho kimefanyika leo tarehe 25 Agosti na kuhudhuriwa na watumishi wa Chuo cha Maji, wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Sehemu ya Uchimbaji Visima, pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja.

Katika kikao hicho, Waziri Aweso ametoa pongezi kwa Chuo cha Maji kwa kazi kubwa inayofanyika na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu. Ameelekeza kwamba mafunzo yote ya kujenga uwezo kwa viongozi wa Wizara ya Maji yafanyike kwenye Chuo cha Maji, kwani Chuo kina wataalamu wa kutosha, vifaa, na miundombinu inayofaa kutoa mafunzo hayo kwa kiwango kinachostahili. Aidha, ameagiza Menejimenti ya Wizara ya Maji ifanye kikao na menejimenti ya Chuo cha Maji ili kuweka mpango wa kuajiri vijana waliohitimu chuo na kuwaingiza kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za Sekta ya Maji.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja, ameeleza kuwa yeye ni mdau mkubwa wa Chuo cha Maji. Amezungumzia jinsi alivyokuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na kuajiri wafanyakazi zaidi ya 1200 kutoka Chuo cha Maji, na pia amewasifu wafanyakazi hao kwa weledi wao kazini na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Chuo cha Maji ili kuendeleza uzalishaji wa wataalamu wenye sifa katika Sekta ya Maji.

Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam O. Karia alimshukuru Waziri wa Maji kwa kutoa mchango mkubwa katika kukiendeleza Chuo, tangu akiwa Naibu Waziri wa Maji mpaka sasa. Aliendelea kumshukuru waziri kwa kumwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hasan Shilingi Bilioni 1.5 za kukarabati mabweni yaliokuwa yamechakaa. Akihitimisha hotuba yake Mkuu wa Chuo aliahidi kutekeleza maagizo aliyotoa Mheshimiwa Waziri na kuendelea kushirikiana na Menejimenti ya Wizara ya Maji kuhakikisha Chuo cha Maji kinakuwa Chuo cha Mfano.

Posted on 26th August, 2023