News

Bodi ya Ushauri Yafanya Ziara Chuo cha Maji, Dar es Salaam

Dar es Salaam, 5 Oktoba 2024 - Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Maji leo wamefanya ziara rasmi katika Chuo cha Maji, Dar es Salaam, ambapo walikagua maendeleo ya miradi mbalimbali. Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kutathmini hatua zilizofikiwa katika ujenzi na ukarabati unaoendelea chuoni ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyokubalika.

Katika ziara hiyo, wajumbe walipata nafasi ya kutembelea jengo jipya la chuo, linalojulikana kama Maji House, ambalo liko katika hatua za mwisho za kukamilika. Wajumbe, wakiwa wameongozana na menejimenti ya chuo, walikagua ofisi na maeneo mengine yaliyopo kwenye jengo hilo jipya ili kupata uelewa wa jinsi litakavyoongeza ufanisi wa shughuli za kiutawala na kimasomo.

Aidha, wajumbe wa bodi walitembelea ujenzi wa maktaba mpya na kuona maendeleo ya ukarabati wa madarasa ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu. Katika ziara hiyo, wajumbe walipata nafasi ya kukutana na mkandarasi anayesimamia mradi huo na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazochelewesha ukamilishaji wa ujenzi huo.

Wajumbe hao walitoa mapendekezo yatakayohakikisha ujenzi huo unakamilika kwa muda uliopangwa na kwa ubora unaohitajika. Miradi hii ya ujenzi na ukarabati itatoa mazingira bora ya kujifunzia na kufanya kazi, na hivyo kuimarisha uwezo wa chuo katika kuzalisha wataalamu wa maji wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye sekta ya Maji.

Posted on 05th November, 2024